Wakazi wa kaunti ya Migori wanaendelea kukadiria madhara ya mvua kubwa inayonyesha magharibi mwa nchi.
Mvua hiyo imesababisha vifo vya watu kadhaa na mali ya maelfu ya pesa kuharibiwa.
Afisa Mkuu wa Mazingira katika kaunti ya Migori Dalmas Odero anasema watu wapatao sita wamefariki kutokana na visa vinavyohusiana na mafuriko.
Odero anasema maeneo yaliyoathiriwa mno ni Nyora na Kabuto yanayopatikana katika eneo bunge la Nyatike.
Afisa huyo sasa ametoa wito kwa familia zinazoishi nyanda za chini kuhamia nyanda za juu ili kuepuka mafuriko.
Serikali ya kaunti ya Migori imechukua hatua za haraka kuwasaidia wakazi katika maeneo yaliyoathiriwa mafuriko.
Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini inasema mvua inatarajiwa kuendelea kunyesha wiki hii katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu za mashariki na magharibi mwa Bonde la Ufa, Ziwa Viktoria na Pwani.