Spika wa Bunge la taifa Moses Wetang’ula amehimiza wapiga kura wa Kaunti ya Meru wamuunge mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, akitaja rekodi ya maendeleo ya serikali hasa katika sekta ya elimu.
Akizungumza wakati wa ibada ya siku ya familia katika Kanisa Katoliki la Mutuati eneo la Igembe Kaskazini, Wetang’ula alisema serikali ya Kenya Kwanza imepiga hatua za kihistoria kwa kuajiri walimu 76,000 tangu iingie madarakani.
Wetangula aliongeza kwamba serikali ina mpango wa kuajiri walimu wengine 24,000 katika bajeti ya sasa.
Aliwataka Wakenya wakatae maandamano ya vurugu na badala yake wazingatie elimu na umoja wa kitaifa akisema kuwa Rais Ruto anastahili muhula wa pili kwa kutimiza ahadi zake.
Spika huyo pia alihakikishia wakazi kuwa serikali inashughulikia suala la usalama katika eneo la Igembe linalokumbwa na wizi wa mifugo, huku akikiri kuwa ukosefu wa ajira ni tatizo la kimataifa ambalo serikali imejizatiti kulikabili.
Alisisitiza kujitolea kwa serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza ahadi za wakati wa kampeni zinazojumuisha kutafuta suluhu kwa tatizo la ukosefu wa ajira ambalo linasababisha uhasama kati ya serikali na raia.
