Wakazi wa Meru wahimizwa kukumbatia utamaduni wao

2 Min Read

Wakazi wa kaunti ya Meru wamehimizwa kukumbatia utamaduni wao kwa ajili ya uendelevu katika vizazi vijavyo. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao cha wanawake wa Meru kuhusu utamaduni mjini Meru, waziri wa zamani wa elimu Jacob Kaimenyi ambaye alikuwa mgeni wa heshima alisema utamaduni una umuhimu wake katika jamii.

Kaimenyi alisema kwamba vijana wengi sasa wamegeukia uraibu wa pombe na aina nyingine za mihadarati kwa sababu wana muda mwingi ambao wangetumia kujifunza utamaduni na kuutekeleza.

Alisisitiza kwamba vitu kama dawa za kienyeji na vyakula vya asili ni muhimu katika kuzuia magonjwa kama kisukari na saratani ambayo yanasumbua watu sana.

Mbunge wa eneo la Imenti Kaskazini Rahim Dawood alikariri maoni sawa na ya Kaimenyi huku akihimiza serikali kuu na zile za kaunti kuchukua hatua za kuendeleza utamaduni wa jamii zote nchini.

Dawood aliomba serikali ya kaunti ya Meru kutenga ardhi ya kujenga kituo cha utamaduni ambacho kitatumiwa na kundi hilo la wanawake na aliahidi kutoa usaidizi katika kuafikia hilo.

Naitore Mugambi, mwenyekiti wa chama hicho cha kina mama wa Meru alisema kwamba waliona ni vyema kuanzisha chama cha utamaduni ili kurejesha na kuboresha utambulisho wa jamii ya Meru.

Alilalamikia hatua ya vijana wengi kuacha kuzingatia utamaduni wao na wanapanga kuandaa matamasha kadhaa ya kitamaduni ili kurekebisha hilo.

Website |  + posts
Jeff Mwangi
Share This Article