Wakazi wa Meru waandamana, wamtaka Gavana Mwangaza aondoke

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Baadhi ya wakazi kaunti ya Meru waliandamana Jumatatu, kushinikiza kuondoka afisi kwa Gavana Kawira Mwangaza.

Maafisa wa Polisi walikuwa na wakati mgumu kuwatawanya waandamanaji hao, waliopinga kurejea afisini kwa Gavana Mwangaza, baada ya Mahakama Kuu kufutilia mbali hatua ya bunge la Seneti kumtimua wadhifani.

Wakazi hao walisema Gavana huyo yuko afisini kinyume cha sheria, hatua iliyowasababisha kuandamana.

Wakazi hao walifunga barabara na kutatiza shughuli za kawaida mjini humo, huku wakisema wamechoshwa na utawala wa gavana Mwangaza.

Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya bunge la Seneti kudumisha hatua ya bunge la kaunti ya Meru ya kumtimua Gavana Mwangaza kwa madai ya utumizi mbaya wa mamlaka, ukiukaji wa sheria na utovu wa nidhamu.

Hata hivyo, uamuzi huo wa bunge la Seneti haukudumu kwa muda mrefu kwa kuwa Gavana huyo alipinga hatua hiyo mahakamani, huku mahakama ikifutilia mbali kutimuliwa kwake na kumrejesha wadhifani.

Wakazi hao wameapa kuendelea na maandamano hayo, hadi Gavana huyo aondoke mamlakani.

Share This Article