Wakazi wa Manguū walalamikia wizi wa vyuma

Daraja muhimu linalounganisha wakazi hao na maeneo muhimu kama shule limeharibiwa na wezi hao.

Marion Bosire
2 Min Read

Wakazi wa mtaa wa mabanda wa Manguū nje ya mji wa Nyahururu katika kaunti ya Laikipia, wamelalamikia wizi uliokithiri wa vyuma na wanabiashara wa vyuma kuu kuu, ulioathiri maeneo ya umma na ya kibinafsi.

Kulingana na mzee wa kijiji Samuel Kamau wezi hao sasa wameanza kuharibu miundombinu ya umma kama daraja la Manguū ambapo wameharibu vifaa vya chuma vilivyokuwepo visa ambavyo hutekelezwa usiku.

Kamau anasema katika muda wa siku chache zilizopita, wameshuhudia uharibifu wa mtambo wa transformer, mifereji ya maji na hata pampu za maji. Waling;oa pia nyaya na kuiba vifaa vya kutumia shambani vilivyoundwa na chuma.

Wanafunzi wa shule ya msingi ya Manguū na wazazi wao walishtuka kuona kwamba daraja la pekee linalounganisha makazi yao na shule limeharibiwa na wanahofia kwamba huenda likaporomoka.

Sasa wanataka maafisa wa usalama wa eneo hilo wachukue hatua za haraka na kukamata wanaotekeleza wizi huo.

Eneo hilo linakabiliwa pia na viboko wanaotoka kwenye eneo la Manguû Sanctuary na kuharibiwa kwa daraja kunaweka wakazi katika hatari.

Januari 2022, serikali ilitangaza kusitishwa kwa biashara ya vyuma kuu kuu nchini kama sehemu ya juhudi za kupambana na wizi wa vyuma kutoka kwa miundomsingi ya umma.

Marufuku hiyo hata hivyo iliondolewa Mei 2022, lakini kanuni mpya zikawekwa hasa ile ya kuhakikisha kwamba ni wafanyabiashara walio na leseni pekee wanaoruhusiwa kutekeleza biashara hiyo.

Maombi ya leseni hizo yalitathminiwa na mashirika ya serikali za kaunti na yeyote ambaye angepatikana akitekeleza biashara bila leseni angefungwa jela au kupigwa faini.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *