Wakazi wa Kampala watakavyokabiliana na msongo wa mawazo

Marion Bosire
2 Min Read

Wakazi wa Kampala jiji kuu la Uganda wamepata namna mpya isiyo ya kawaida ya kukabiliana na msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za maisha ya sasa.

Wamebuni kundi moja la wapiga nduru yaani “The Kampala Scream Club” ambalo sasa linaalika wakazi walio na msongo wa mawazo katika maeneo ya wazi ambapo watakuwa wanapiga nduru kila mmoja ili kutoa mawazo yaliyojaa ndani yao.

Awamu ya kwanza ya mpango huo wa kupiga nduru ilifanyika jana Jumapili Oktoba 12, katika kilima cha Buziga, ambapo waandaaji walihakikishia wahusika usalama na eneo ambapo hawatahukumiwa na yeyote.

Katika ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti rasmi ya Instagram, kundi hilo lilihimiza washiriki likisema “Tunaishi katika ulimwengu unaotuhimiza kusalia kimya, tuyashikilie kwa ndani na kujifanya tuko sawa huku msongo wa mawazo, hasira, kiwewe na hata furaha isiyosemeka vikitujaa ndani”.

Wahusika walielezewa kuhusu watakayoyafanya katika eneo hilo ambayo sanasana yanahusu kupiga nduru na hata kufoka ili kuondoa msongo wa mawazo na hisia na kufanya upya mwili na akili.

Waandalizi wanasema lengo lao kuu ni kuunda utu wa pamoja kwani wahusika watagundua kwamba sio wao pekee waliobeba mizigo mizito kimawazo na kwamba sio lazima waendelee kuibeba.

Tangazo hilo liliibua mjadala kati ya wanamitandao nchini Uganda wengi wakikosa kuamini iwapo namna hiyo ni faafu katika kukabiliana na msongo wa mawazo.

Wakosoaji wanahisi kwamba namna hiyo ni ya wazungu na haiambatani na namna za kitamaduni na tamaduni za uponyaji.

Website |  + posts
Share This Article