Wakazi na wamiliki wa biashara katika Kituo cha Biashara cha Boiman, eneo la Gathanji, Eneo Bunge la Ol-Joro Orok, kaunti ya Nyandarua, wameandamana kulalamikia ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Wameripoti ongezeko la matukio ya wizi na uvamizi wa maduka, mengi yakiwa yametokea karibu kabisa na Kituo cha Polisi cha Boiman. Waandamanaji wamewalaumu maafisa wa polisi wa eneo hilo kwa uzembe na kutochukua hatua, na wanaitaka serikali kuwahamisha mara moja.
John Rukungu, ambaye ni mmoja wa waathiriwa wa hivi karibuni, alisema duka lake la vifaa vya elektroniki liliingiliwa na bidhaa zenye thamani ya zaidi ya KSh 200,000 kuibiwa.
Alieleza kuwa alifahamishwa kuhusu tukio hilo na alipofika eneo hilo kwa haraka, alikuta milango ya duka lake imevunjwa kwa nguvu. Wahalifu hao walizima na kuzuia kamera za CCTV kabla ya kuingia na pia waliharibu kioo cha kuonesha kamera hizo.
Wafanyabiashara wenzake, Zachary Kimani na James Njenga, pia walieleza kuchoshwa kwao na hali hiyo, wakidai kuwa wahalifu hao hawaogopi kutekeleza uhalifu hata karibu na kituo cha polisi.
Walieleza wasiwasi wao kuwa huenda baadhi ya maafisa wa polisi wanashirikiana na wahalifu.
Wakazi pia walilalamikia kuwa taa ya usalama ya mlingoti mrefu, iliyowekwa na Serikali ya Kaunti ya Nyandarua umbali wa mita 20 tu kutoka eneo la tukio, haifanyi kazi — pamoja na taa za barabarani zilizokaribu — hali inayofanya eneo hilo kuwa hatarishi wakati wa usiku.
Maandamano hayo yaliendelea kwa muda mrefu wa siku nzima, huku wamiliki wa biashara wakifunga maduka yao ili kushiriki maandamano hayo. Walitoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka.
Chifu Mkuu wa Eneo la Huhoini, Samwel Kinyanjui, alizuru eneo hilo katika juhudi za kuwatuliza waandamanaji. Aliwahakikishia kuwa uchunguzi unaendelea na yeyote atakayepatikana akishirikiana na wahalifu atachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, alithibitisha kuwa suala hilo tayari limeripotiwa kwa timu ya usalama ya Kaunti na akasisitiza kuwa serikali imejitolea kuhakikisha usalama wa wakazi na biashara zao.