Wakenya wamehimizwa kuwakumbatia wafungwa katika jamii, wanapokamilisha muda wa kifungo chao.
Waadau katika idara ya urekebishaji tabia, walidokeza kuwa baadhi ya wanaokamilisha kifungo, hukamatwa na kurejeshwa tena gerezani kutokana na kutengwa na jamii na unyanyapaa.
Katibu katika idara ya urekebishaji tabia katika wizara ya usalama wa taifa Salome Muhia, alisema idara ya magereza imeanzisha mipango ya kuwawezesha wanaokamilisha kifungo cha gerezani kuwa na uwezo wa kujitegemea katika jamii.
“Tuwasaidie wafungwa ili wanapoachiliwa, hawakamatwi tena na kurejeshwa gerezani. Wakaribisheni tena katika jamii,”alisema katibu huyo.
Aidha katibu huyo alitoa wito kwa washirika zaidi kuunga mkono idara ya urekebishaji tabia hapa nchini, kupitia utoaji ushauri nasaha.
“Ikiwa wewe ni mtaalam wa utoaji ushauri nasaha, wasiliana nasi, njoo uwasaidie wafungwa kubadili tabia. Tushirikiane kuwasaidia watu wetu,”alisema Muhia.
Katibu huyo aliyasema hayo alipozuru gereza la Nanyuki katika kaunti ya Laikipia, kabla ya kuzindua ujenzi wa kituo mafunzo kilichofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Faraja.