Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum nchini Tanzania Dorothy Gwajima amekemea vikali ongezeko la maudhui yasiyofaa yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Gwajima alitoa mfano wa mtengeneza maudhui mmoja ambaye hivi karibuni ameonekana akisambaza maudhui ya kuuza figo za mtoto, mwingine akaonyesha maudhui ya kuandaa vinywaji na vyakula vichafu akijigamba kwamba anauzia watu wa Kariakoo na wa maeneo mengine.
Maudhui mengine aliyoyakemewa Waziri Gwajima ni ya wale wanaosambaza maudhui ya kufanya mapenzi hadharani yakiwemo ya jinsia moja, wengine wakisambaza maudhui kuhusu fursa za kujipatia fedha kwa njia zisizoeleweka.
Waziri Gwajima amewataka watengeneza maudhui kuzingatia weledi na miongozo yote na kama mtu hana elimu na ufahamu kuhusu kuandaa maudhui ya mitandaoni aache mara moja.
Alionya kwamba kila mmoja wao atawajibishwa binafsi kwa kuandaa maudhui ambayo yanachukuliwa kuwa kinyume na maadili ya taifa hilo la Afrika Mashariki.