Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru, ametajwa kuwa tayari kuongoza wadhifa wa kitaifa katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Waiguru, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana, ametajwa kuwa kiongozi mwenye kuleta mabadiliko, ambaye kazi yake katika kaunti ya Kirinyaga ni ya kupigiwa mfano.
Hayo yalisemwa na viongozi wanawake kwenye kongmano la G7, lililoandaliwa Alhamisi katika kaunti ya Kirinyaga.
Baadhi ya viongozi wanawake walimhimiza gavana huyo, awanie wadhifa wa urais hapa nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, alidokeza kuwa Waiguru amewahudumia wakazi wa Kirinyaga kwa kujitolea kikamilifu, na sasa anapaswa kuwahudumia wananchi katika ngazi ya kitaifa
“Waiguru ni mjasiri, na anafaa kwa wadhifa wa kitaifa,” alisema Wanga.
Wanga aliongeza kuwa viongozi wenzake wanawake, wamejifunza mengi kutoka kwa Waiguru, na urithi wake utadumu milele.
Matamshi ya Wanga yaliungwa mkono na mwenzake wa Machakos Wavinya Ndeti, aliyesema atatekeleza baadhi ya miradi ambayo yamefanywa katika kaunti ya Kirinyaga.
“Gavana Waiguru aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa Gavana hp nchini, na kutuptia motisha ya kuwania wadhifa huo. Tunamuunga mkono anapozidi kuwahimiza wanawake zaidi kuwania nyadhifa za uongozi,” alisema Ndeti.
Waiguru, aliyeandaa kikao hicho pamoja na wenzake Fatuma Achani wa Kwale, Wavinya Ndeti wa Machakos na Gladys Wanga wa Homa Bay anataka wanawake zaidi wajiunge kwenye uongozi na kutetea usawa wa kijinsia na uongozi jumuishi.
Mkakati wa G7 ulioanzishwa mwezi Machi mwaka huu unanuia kuwapa uwezo na kuwaunga mkono wanawake viongozi ili kudhihirisha uongozi bora na wa kuleta mabadiliko.
Kadhalika unatilia mkazo kuwapa wanawake uwezo wa kiuchumi.