Wabunifu wengi wakiwemo waigizaji nawachekeshaji na wengine katika sekta ya burudani walikongamana jana katika jumba la KICC kuunga mkono mwenzao Kennedy Odhiambo maarufu kama Crazy Kennar.
Onyesho hilo la kwanza jukwaani kwa mchekeshaji huyo wa mitandaoni lilipatiwa jina la “Happy Country”.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa onyesho, Jackie Vike ambaye nafahamika sana kama Awinja alisema Kennar amewamotisha sana kwa hatua ambayo alichukua ya kubadili kutoka kwa vipindi vilivyorekodiwa hadi onyesho la moja kwa moja jukwaani.
Alihimiza watu kwa jumla wasiwekee waigizaji na wachekeshaji mipaka kutokana na jinsi watu walitilia shaka uwezo wa Kennar kutumbuiza jukwaani alipotangaza ujio wa onyesho lake.
Huku akisema naye atapanga onyesho lake siku za usoni, Vike alisema kwamba yeye ana uwezo wa kutekeleza majukumu yote ya uigizaji.
Eddie Butita aliwarushia maneno waliokosa kumwamini Kennar ambapo aliwahimiza waendelee kumchukia huku akitengeneza pesa.
Jackie Matubia ambaye wengi walipata kumfahamu kupitia kipindi cha Tahidi High ambapo alikuwa akiigiza kama Joylyn alikiri kutofahamiana na Kennar mmoja kwa moja lakini anafahamu kazi yake na alinunua tikiti ya onyesho hilo kama njia ya kumuunga mkono.
Alihimiza wabunifu kuunga mkono wenzao wanapopanga maonyesho kama hayo huku akiwaomba wasiwe na chuki dhidi ya wanaojiunga na tasnia na wanaonekana kufanikiwa zaidi ya walioanza zamani.