Wahusika wa mauaji ya Muchai wahukumiwa kifo

Wengine wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani huku mmoja akiondolewa mashtaka.

Marion Bosire
1 Min Read

Washtakiwa wa kwanza wanne waliopatikana na hatia ya wizi wa kimabavu uliosababisha mauaji ya aliyekuwa mbunge wa Kabete George Muchai wamehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama ya Milimani.

Wanne hao Eric Muyera Isambwa, Raphael Kimani Gachii, Mustapha Kimani Anyoni na Stephen Astiva Lipopo, wanakabiliwa pia na shtaka jingine la mauaji katika mahakama kuu.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Mkuu Lucas Onyina, aliwapa washtakiwa wa 5 na 6th Jane Wanjiru Kamau na Margaret Njeri Wachiuri kifungo cha miaka 10 gerezani, muda utakaohesabiwa kuanzia wakati waliwekwa rumande kwa mara ya kwanza baada ya kukamatwa.

Wanawake hao wawili walipatikana na makosa madogo madogo kama kumiliki silaha kinyume cha sheria, katika kesi hiyo iliyodumu zaidi ya miaka 10 na iliyokuwa na mashahidi 37.

George Muchai ambaye alikuwa mtetezi shupavu wa wafanyakazi na mwanasiasa, aliuwawa kwa kupigwa risasi Februari 7, 2015 wakati yeye na watu wa familia yake walikuwa wanaelekea nyumbani baada ya kupata chajio.

Gari lake liligongwa na gari jingine kisha washambulizi hao wakatoka kwenye gari husika na kumpiga risasi na kumuua yeye, walinzi wake wawili na dereva.

Share This Article