Wahudumu wa Bodaboda, wamehimizwa kuwa katika mstari wa mbele kuwasaidia maafisa wa polisi kukabiliana na uhalifu mjini Narok.
Gavana wa kaunti ya Narok Patrick Ole Ntutu, alisema wahudumu hao wana jukumu kubwa la kutekeleza, kuhakikisha asasi za usalama zinapata habari kuhusu visa vya utovu wa usalama katika eneo hilo.
Kulingana na Gavana huyo, watu wengi wamedhulumiwa na majambazi mjini Narok, wengi wa majambazi hao wakijisingizia kuwa wahudumu wa bodaboda.
Aliwataka wahudumu hao wa bodaboda kuhakikisha wateja wao wanawasili nyumbani salama, huku akiwaonya dhidi ya kuwaibia wateja wao.
Aidha Gavana huyo alilalamika kuwa idadi kubwa ya visa vya mimba za mapema, vinasababishwa na wahudumu wa bodaboda, ambapo aliwaonya dhidi ya kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi wa wasichana wa shule.
Kamishna wa kaunti ya Narok Isaac Masinde, kwa upande wake, alithibitisha kuwa amri ya kutohudumu kwa sehemu za burudani kuanzia saa nne usiku ingalipo.
Kamishna huyo wa kaunti alidokeza kuwa viongozi wa kidini na wafanyabiashara wamekuwa wakimsihi kuondolea mbali makataa hayo, lakini akadokeza kuwa hatabatilisha amri hiyo.
Masinde aliwaonya wahudumu hao wa bodaboda dhidi ya kujihusisha na vitendo vya uvunjaji wa sheria.