Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jana alitangaza msamaha kwa wafungwa 4,887 ambapo 42 kati yao waliachiliwa huru jana Aprili 26, 2025.
Wafungwa wengine 4,845 walihitajika kukamilisha taratibu muhimu za vifungo vyao baada ya kupatiwa msamaha na wataondoka baadaye.
Taarifa ya serikali kupitia wizara ya mambo ya ndani nchini Tanzania ilielezea kwamba msamaha huo wa Rais Samia ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya muungano wa Tanzania.
“Ni matarajio ya Serikali kuwa Wafungwa hao watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa letu na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani” ilisema taarifa hiyo.
Miongoni mwa wanaonufaika na msamaha huo ni wafungwa waliohukumiwa kifo kwa njia ya kunyongwa waliomaliza taratibu za mahakama ambapo wanabadilishiwa adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha.
Chini ya taratibu za msamaha huo, adhabu ya kifungo cha maisha gerezani pia inabadilishwa na kuwa Kifungo cha miaka 30 gerezani.
Wengine wanaopata msamaha ni Wafungwa wazee wa umri wa miaka 70 na zaidi ambao wamehukumiwa kifungo cha muda maalum na waliokaa gerezani kwa muda wa miaka miwili na zaidi.
Wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito au walioingia na watoto wanaonyonya, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na matatizo ya afya ya akili wasio na uwezo wa kufanya kazi pia watanufaika na msamaha huo wa Rais Samia.