Wafanyazaki kuelemewa na mzigo wa ushuru, asema Okwaro

Dismas Otuke
1 Min Read

Naibu katibu mkuu wa muungano wa wafanyakazi nchini, COTU Benson Okwaro amesema ushuru unaotozwa na ule unaopangwa kuanzishwa na serikali utakuwa mzigo mkubwa kwa wafanyakazi wote nchini.

Kwenye mahojiano ya kipekee na shirika la KBC, Okwaro ametaja matozo ya NSSF, matozo ya nyumba, nyongeza iliyopangwa ya ushuru wa thamani ya ziada kutoka asilimia 16 hadi 18 na matozo yaliyopendekezwa kugharimia wasio na ajira akisema huenda yakawaacha hoi bin taabani wafanyakazi wanaotegemea mishahara kwani huenda wakakosa kujikimu.

Okwaro ambaye pia ni katibu mkuu wa chama cha wafanyikazi wa sekta ya mawasiliano nchini, COWU badala yake amependekeza serikali itafute njia nyingine mbadala za kugharimia matumizi yake badala ya kulimbikiza mzigo wote kwa wale walio na ajira.

Matamshi ya Okwaro yanajiri wakati ambapo Wakenya wengi wanalalamikia gharama ya juu ya maisha ambayo inaendelea kuwa ghali zaidi kila kuchao tangu ujio wa serikali mpya ya Kenya Kwanza.

Katibu huyo mkuu pia amekiri kuwa huenda ikawa vigumu zaidi kupigania nyongeza mpya ya mishahara ya wafanyakazi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na mfumko wa bei unaoshuhudiwa na usiotabirika.

Share This Article