Wafanyikazi 108 katika afisi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, walioshurutishwa kwenda likizo wametakiwa kuwasilisha nakala za kandarasi za ajira zao mahakamani.
Jaji wa mahakama ya uajiri na maswala ya wafanyikazi Hellen Wasilwa, anayesikiza kesi hiyo,amewataka wafanyikazi hao 108 kuambatanisha mikataba yao ya kazi kwenye faili ya kesi.
Jaji Wasilwa pia amewapa washtakiwa wa kwenye kesi hiyo wakiwemo Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Kosgei, muda wa siku saba kuwasilisha utetezi wao.
Kesi hiyo iliyowasilishwa na Wakili wa wafanyikazi Lempaa Suiyanka ambayo itaskizwa Novemba 13, inapinga jinsi wafanyikazi hao walivyoshurutishwa kwenda likizo baada ya kubanduliwa afisini kwa Gachagua.
Katibu Mwandamizi katika afisi ya Naibu Rais Partick Mwangi, aliwaagiza wafanyikazi waote wa afisi ya Naibu Rais kwenda kwa Likizo ya lazima Oktoba 18 .