Wafanyakazi wawili wa KQ waliokuwa wakizuiliwa DRC waachiliwa huru

Tom Mathinji
1 Min Read

Shirika la ndege la Kenya Airways KQ, limetangaza kuachiliwa huru kwa wafanyakazi wake wawili, waliokuwa wakizuiliwa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Kupitia kwa taarifa, afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Allan kilavuka, alisema wafanyakazi hao wawili waliokuwa wakishikiliwa na maafisa wa jeshi, waliachiliwa bila masharti yoyote.

“Shirika la Kenya Airways linathibitisha kuwa maafisa wa kijeshi Jijini Kinshasa, wamewaachilia huru wafanyakazi wetu wawili waliokuwa wakizuiliwa tangu Aprili 19, 2024,” alidokeza Kilavuka

Kilavuka alishikilia kuwa maafisa hao hawakuwa na hatia yoyote, ila tu walikuwa wakitekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kikamilifu sheria zilizopo.

“Tunashikilia kuwa hawakuwa na hatia yoyote, na tutaendelea kuwaunga mkono,” alisema Kilavuka.

kufuatia hatua hiyo, shirika hilo limetangaza kurejelewa kwa safari za ndege kati ya Nairobi na Kinshasa kuanzia Mei 8, 2024.

“Tunatangaza kurejelewa kwa safari za ndege Jijini Kinshasa tarehe 8 mwezi Mei,” Lilisema shirika hilo.

Kilavuka alimshukuru waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi, serikali ya Kenya na wafanyakazi wa shirika hilo Jijini Kinshasa na Nairobi, kwa juhudi walilotekeleza kuhakikisha maafisa hao wanaachiliwa huru.

Wafanyakazi hao wawili walikamatwa na maafisa wa jeshi kufuatia mzozo wa stakabadhi wa mzigo katika uwanja wa ndege wa Kinshasa.

Share This Article