Wafanyakazi wa serikali ya kaunti ya Embu wasimamishwa kazi kuhusiana na kisa cha moto

Marion Bosire
2 Min Read

Wafanyikazi watano wa serikali ya kaunti ya Embu idara ya zimamoto, wamesimamishwa kazi kwa kile kinachosemekana kuwa kukosa kutoa huduma wakati wa dharura, moto ulipozuka Jumatano katika eneo la makazi la Majengo mjini Embu. Moto huo ulisababisha familia 8 kupoteza makazi.

Mkurugenzi wa afisi ya maswala ya majanga na dharura na wahudumu wa kuzima moto waliokuwa kwenye zamu siku hiyo ndio wamesimamishwa kazi wakisubiri uchunguzi ili kufahamu utepetevu kwa upande wao kulingana na Gavana Cecily Mbarire.

Mbarire aliomba msamaha waathiriwa wa mkasa huo kufuatia hatua ya wahudumu wa kuzima moto ya kukosa kufika mahala pa mkasa siku hiyo hata kama afisi zao ziko umbali wa kilomita tatu tu kutoka eneo hilo, na walikuwa na vifaa stahiki vya kuzima moto.

Gavana huyo alijuta kwamba usaidizi ulitoka kwa kaunti jiani ya Kirinyaga ambayo ilituma gari la kuzima moto ilhali wahudumu wake hata hawakwenda kuwasaidia.

Bi. Mbarire ameamuru maafisa husika wampe ripoti kamili kuhusu hali ya magari ya kuzima moto yanayomilikiwa na serikali ya kaunti ya Embu akisema walichokifanya wahudumu hao wa kuzima moto ni hujuma na atachunguza na kuchukua hatua inayostahili.

Mwakilishi wa wadi ya Kirimari Ibrahim Swale alishukuru Gavana Mbarire kwa hatua ambayo amechukua. Awali, Swale alikuwa ametaka Gavana awafute kazi wahudumu wote wa idara ya kuzima moto.

Kulingana naye, hatua itakayochukuliwa dhidi ya waliozembea kazini itakuwa funzo na onyo kwa watendakazi wa umma ili wajiepushe na vitendo kama hivyo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *