Wafanyakazi wa KPA waonywa dhidi ya ufisadi

Martin Mwanje
1 Min Read
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amewaonya wafanyakazi wa Halmashauri ya Bandari Nchini, KPA dhidi ya kujihusisha katika ufisadi. 
Akiwahutubia wafanyakazi na timu ya wasimamizi wa KPA katika makao makuu ya halmashauri hiyo huko Kilindini, Mombasa, Koskei aliwaonya wafanyakazi watakaopatikana katika visa vya ufisadi akisema watawajibikia vitendo vyao.
“Hakuna kitu kama maagizo kutoka juu,” alionya Koskei katika mkutano uliohudhuriwa na mwenyekiti wa bodi ya KPA Benjamin Tayari na Mkurugenzi Mkuu, Kapteni William Ruto.
Koskei alisema KPA ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi na kwa sababu hiyo, serikali iko makini kuhakikisha ina rasilimali za kutosha ili kuboresha utendakazi wake.
Alipongeza usimamizi wa halmashauri hiyo, wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi kwa kufanya kazi kwa amani, mafanikio aliyosema yataifanya bandari hiyo kubwa zaidi Afrika Mashariki kufikia upeo wa maendeleo.
Mapema, Koskei aliwatembelea Kamishna wa Kanda ya Pwani Rodah Onyancha na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Ahmed Shariff.
Kisha alikagua hatua iliyopigwa katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu na mradi wa Gesi wa Taifa.
Koskei yupo kwenye ziara ya siku tatu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika eneo la pwani iliyoanza Julai 4, 2023 kwa kutembelea mradi wa wsalama wa Chakula wa Galana Kulalu.
Website |  + posts
Share This Article