Wafanyakazi kupata asilimia sita ya nyongeza ya mshahara

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais William Ruto ameitaka Wizara ya Leba kufanya mkutano na kamati husika ya uhusiano wa wafanyikazi ili kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa angalau asilimia sita.

Hii, alisema, ni sehemu ya mpango wa serikali kuinua masilahi ya wafanyikazi.

Rais Ruto pia aliagiza Wizara ya Kazi na Ulinzi wa Jamii kutekeleza mabaraza mengi ya mishahara yaliyotolewa na Sheria ya Mahusiano ya Kazi ya 2007, ikilenga kuhakikisha amani ya kiviwanda na udhibiti mzuri wa mizozo.

Hizi ni pamoja na mabaraza ya mishahara kwa mabaharia na wafanyikazi wa ulinzi, wafanyikazi wa kawaida na wa kilimo.

“Watajadili kima cha chini cha mishahara katika sekta tofauti, kuimarisha upatanishi na amani ya viwanda,” alisema.

Rais Ruto alisema hayo wakati wa sherehe za 59 za Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi katika Uwanja wa Kitaifa wa Uhuru Gardens, Kaunti ya Nairobi.

Rais alisema serikali inafanya kila iwezalo kukuza uchumi na kuhakikisha ustawi wa wananchi wote.

Alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kusimamia mfumuko wa bei, kuleta utulivu wa sarafu na kushughulikia madeni.

“Sera zetu za kiuchumi pia zimepunguza bei ya bidhaa za kimsingi, na kupunguza shinikizo kwa wafanyikazi,” alisema.

Rais alisema serikali ina mpango wa makusudi wa jinsi ya kuunda nafasi za kazi, akitaja mpango wa nyumba za bei nafuu, vituo vya kidijitali na kazi za nje ya nchi.

Aliwataka madaktari kusitisha mgomo wao na kufanya mazungumzo na serikali kwa nia njema.

Rais alisema ingawa madaktari wana haki ya kufanya migomo, jambo hilo linapaswa kufanyika kwa uwajibikaji na kwa kuzingatia ustawi wa wananchi.

Viongozi waliohudhuria ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Leba Florence Bore, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli, miongoni mwa wengine.

Share This Article