Wafanyabiashara zaidiya 1,000 katika soko la Githurai 45, kaunti ndogo ya Ruiru kaunti ya Kiambu, hatimaye wameingia katika soko jipya la Githurai.
Hafla hiyo iliongozwa na waziri wa biashara wa kaunti hiyo Susan Gatwiri, na afisa mkuu wa kaunti hiyo Simon Kiberenge.
Awali Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi alipongeza uwazi na uwajibikaji wakati wa ugawaji wa soko hilo kwa wanabiashara hao.
“Tuliwaahidi kuwa tutatekeleza mchakato wa ugawaji soko hilo kwa wafanyabiashara kwa njia iliyo wazi na usawa,” alisema Wamatangi.
Soko hilo lililojengwa kwa kitita cha shilingi milioni 400 na lililo na uwezo wa kuwahifadhi wafanyabiashara 1,200, lilifunguliwa rasmi Agosti 4,2023 na Rais William Ruto.
Wakati wa ufunguzi huo, Rais Ruto alitoa wito kwa Gavana wa Kiambu kushughulikia maslahi ya wafanyabishara waliokuwa kando kando ya barabara.