Waendeshaji pikipiki za uchukuzi wa abiria almaarufu bodaboda katika kaunti ya Meru wamehamasishwa kuhusu usalama barabarani na kupata ujuzi wa huduma ya kwanza iwapo ajali zitatokea wakati tunakaribia msimu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya.
Kundi moja kwa jina “Youths for Boy Child” limekuwa likizuru stendi mbali mbali za pikipiki hizo za uchukuzi wa abiria katika kaunti ya Meru kuhamasisha waendeshaji.
Mwanzilishi wa kundi hilo Kenton Muthethia anasema lengo lao ni kuhakikisha kwamba ajali ambazo hushushudiwa wakati wa sherehe za mwisho na mwanzo wa mwaka zinapungua pakubwa.
Kundi hilo linagawia waendeshaji bodaboda hao mavazi ya kujihakikishia usalama huku wakiombwa kufuata kanuni zote za usalama barabarani.
Patrick Mwangi mkurugenzi wa shule ya mafunzo ya uendeshaji magari naye aliwataka waendeshaji hao kutii sheria za barabarani na wahakikishe wana leseni za uendeshaji.
Julius Thiaine mwendeshaji bodaboda katika eneo la Ncheru katika kaunti ndogo ya Tigania Magharibi alipongeza juhudi za kundi hilo la vijana akisema wengi wa waendeshaji hawafahamu sheria za trafiki.
Anaitaka serikali kuhakikisha uendelevu wa uhamasisho kama huo huku akiomba watumiaji wote wa barabara kuwa makini.