Wadau Nairobi watakiwa kushughulikia changamoto zinazozuia upatikanaji haki

Tom Mathinji
1 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome.

Jaji Mkuu Martha Koome ametoa wito kwa serikali ya taifa, ile ya kaunti ya Nairobi na wadau wengine, kushirikiana ili kutatua vizingiti dhidi ya upatikanaji haki eneo la Nairobi.

Akizungumza leo Ijumaa wakati wa uzinduzi wa mahakama ya Dagoretti katika kaunti ya Nairobi, Jaji huyo Mkuu alisema juhudi za kuhakikisha upatikanaji haki na huduma za idara ya mahakama katika kaunti ya Nairobi, zinakumbwa na changamoto kuu, haswa kutoka na idadi kubwa ya watu, ukuaji wa haraka na idadi ndogo ya mahakama miongoni mwa maswala mengine.

“Idara ya Mahakama inashughulikia idadi kubwa ya kesi kaunti ya Nairobi, pamoja na kaunti jirani kama vile Kiambu, Machakos,na Kajiado, ambazo huchukua thuluji moja ya kesi zote,” alisema Koome.

Kulingana na Koome, kaunti ya Nairobi ikiwa na idadi ya watu Milioni 5.5 ambayo ni asilimia 10 ya idadi jumla ya taifa, idadi ya kesi zinazowasilishwa ni ya juu zaidi.

“Hatujawekeza zaidi katika miundombinu ya mahakama kuambatana na idadi ya watu  inayoongezeka kaunti ya Nairobi,” aliongeza Jaji huyo Mkuu.

Mahakama hiyo mpya ya Dagoretti inatarajiwa kushughulikia kesi ndogo ndogo na kesi za jinsia na hivyo kupunguza msongamano katika mahakama za Kibra na Kikuyu.

TAGGED:
Share This Article