Wadau wa tasnia ya uigizaji ya Hollywood wanaendelea kutoa jumbe zao za kumkumbuka mwigizaji Diane Keaton aliyefariki akiwa na umri wa miaka 79.
Gwiji huyo wa uigizaji alifariki Jumamosi Oktoba 11 huko California ila hakuna taarifa zaidi kuhusu mazingira ya kifo hicho huku familia yake ikiomba ufaragha.
Idara ya zima moto ya Los Angeles ilithibitisha kwamba maafisa wake walijibu wito nyumbani kwa Diane na kumsafirisha hadi hospitali alikofia.
Jane Fonda ambaye aliigiza na Keaton kwenye filamu Book Club alimtaja kuwa nyota ya uzima na mwanga katika ujumbe wake wa kumwomboleza, akiendelea kusema kwamba ni vigumu kuamini na kukubali kwamba amefariki.
Bette Midler ambaye aliigiza na Keaton mwaka 1996 katika first Wives Club aliandika haya kwenye Instagram, “Diane Keaton mwerevu, mrembo na asiye wa kawaida amefariki. Siwezi kuelezea jinsi hili linanitamausha.”
Aliendelea kwa kukumbuka Diane alivyokuwa mcheshi, asilia na mkamilifu na kwamba ulivyomwona ndivyo alivyo.
Goldie Hawn ambaye pia aliigiza na Diane kwenye First Wives Club aliandika, “Diane, hatuko tayari kukupoteza. Umetuachia vumbi iliyo na chembechembe za mwanga na kumbukumbu zinazozidi mawazo yetu.”
Steve Martin ambaye aliigiza kama mume wa Keaton kwenye filamu Father of the Bride alimuenzi Keaton kwenye Instagram,ambapo alichapisha picha ya maswali na majibu wakiwa na mwenzao Martin Short kwenye mahojiano mwaka 2021.
Viola Davis kwa upande wake alidhihirisha jinzi alibyoumizwa na taarifa za kifo cha Diane Keaton ambapo aliandika, “Hapana!! Hapana!!! Hapana!! Mungu, bado, Hapana!!! Yaani uliupa uanamke maana”
Aliendelea kuorodhesha majukumu aliyoigiza wakati wa uhai wake ambapo alichukulia kila jukumu kwa uzito na kuliweka moyoni akimalizia kwa kumtaka alale salama na Mungu abariki familia yake.
Mandy Moore aliyeigiza na Keaton kama binti yake kwenye igizo la vichekesho la mwaka 2007 liitwalo Because I Said So naye alichapisha ujumbe wa buriani kwenye Instagram.
Alichapisha picha kutoka kwenye igizo hilo na kuandika, “Walisema usikutane na shujaa lakini mimi nilipata fursa ya kufanya kazi na wangu na hata nikamwita mama kwa miezi kadhaa”.