Wabunifu wa mtandaoni kupokea malipo kuanzia mwezi Juni

Tom Mathinji, PCS, PCS and PCS
3 Min Read
Rais Ruto akutana na wawakilishi wa Meta katika Ikulu ya Nairobi.

Wasanii wa mtandaoni hapa nchini wana sababu ya kutabasamu, baada ya serikali kutangaza kuwa wataanza kupokea mapato kutokana na kazi zao kwenye Facebook na Instagram kufikia Juni mwaka huu.

Hatua hiyo inaifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazofurahia fursa hiyo.

Hatua hiyo ilitangazwa na Rais wa masuala ya kimataifa wa Facebook, Nick Clegg, katika mkutano na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Tangazo hilo ni hitimisho la msukumo wa mwaka mzima wa serikali unaoongozwa na rais kutaka wabunifu wapate mapato kutokana na kazi za sanaa za mtandaoni.

“Wabunifu wa mtandaoni wa Kenya ambao wanakidhi vigezo vya kustahiki, sasa watapata mapato kutokana na nafasi zao za Facebook na Instagram tunapoanza uchumaji wa mapato kufikia Juni mwaka huu,” Bw Nick alisema.

Rais William Ruto alisifu ushirikiano kati ya Kenya na mifumo ya kimataifa ya kidijitali kuhusu uchumaji wa kazi za sanaa.

“Sasa wabunifu wa mtandaoni wanaweza kuanza kuchuma mapato kutokana na mawazo na ubunifu wao. Nimetimiza ahadi yangu ya kujadiliana na kupata fursa mpya,”

“Ushirikiano wetu kati ya Kenya, Meta na Facebook unalenga kupanua fursa kwa vijana. Tunaendeleza mashauriano yetu ili kutafuta fursa zaidi kwa vijana kupitia kuunda maudhui,” alisema.

Aliongeza: “Tuna uhakika na nafasi ya kidijitali kuunda nafasi za kazi kwa mamilioni ya vijana wasio na kazi katika nchi yetu.”

Kiongozi wa Nchi alibainisha kuwa uanzishwaji wa uchumi thabiti wa ubunifu unasalia kuwa kipaumbele cha serikali kulingana na Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya kutoka Chini kwenda Juu.

Alisema ni kupitia ushirikiano na majukwaa ya kidijitali ya kimataifa ambapo vijana wanaweza kupata fursa ya kutumia vipaji vyao.

Rais Ruto alikaribisha mipango ya kuwa na uchumaji wa mapato kwa M-Pesa.

“Nina furaha kwamba timu ya Meta tayari imefanya jaribio la kuchuma mapato kwenye M-Pesa. Jaribio hilo lilionyesha kuwa linafanya kazi. Hii itawezesha wabunifu kutumia fursa hiyo,” alisema Rais Ruto.

Alisema serikali inafanyia kazi upya sheria ili kurahisisha wageni kufanya kazi na wenyeji hasa kwenye majukwaa ya kidijitali.

Alisisitiza juu ya haja ya majukwaa ya kidijitali ya kimataifa kuwa na kazi za sanaa ambazo haziwezi kutumiwa vibaya.

Bw Clegg alisema tasnia ya ubunifu imeunda nafasi nyingi za kazi kwa vijana.

Aliwataka Wakenya kunufaika na hatua hiyo ya kuchuma mapato ya Facebook ili kupata pesa zaidi za kuboresha maisha yao.

Bw Clegg alisema kuwa Facebook ilikuwa na nia ya kufanya kazi na Kenya kuwekeza kwa watu ili waweze kujua jinsi ya kutumia zana za uchumaji mapato kwa manufaa yao wenyewe.

Waziri wa Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (ICT) Eliud Owalo alisema wizara yake itahakikisha mazingira mazuri kwa ubunifu wa sanaa kustawi nchini.

Website |  + posts
Share This Article