Wabunge waelezea hofu kuhusu makaburi ya Lang’ata

Marion Bosire
1 Min Read

Wabunge sasa wanaitaka Wizara ya Afya itathmini hatari za kiafya zinazotokana na matumizi endelevu ya eneo la makaburi la Lang’ata, zaidi ya miaka 10 tangu eneo hilo kutangazwa kuwa limejaa.

Viongozi hao walikuwa wakichangia mjadala wa mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor, ambapo waliitaka serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Nairobi zitafute eneo mbadala la maziko.

Oduor anasema hatua ya watu kuendelea kutumia eneo hilo imesababisha lijae kupita kiasi na wakati mwingine wengine wanapatiwa eneo ambalo tayari limetumika.

Kutokana na hilo, miili ambayo wenyewe wanalazimika kuizika kwenye makaburi ya kina kifupi hufukuliwa kila mara na wanyama kutoka mbuga iliyo karibu.

Mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi aliunga mkono mjadala huo huku akiomba serikali ya kaunti ya Nairobi itenge fedha za kusaidia kumaliza tatizo hilo.

Alielezea kwamba wakati alikuwa akihudumu kama diwani katika iliyokuwa manispaa ya jiji la Nairobi, walitenga pesa za kununua ardhi nyingine ya makaburi lakini fedha hizo zikafujwa.

Eneo la makaburi la Lang’ata ndilo eneo kubwa la maziko jijini Nairobi na limetumika tangu mwaka 1958.

Ongezeko la idadi ya watu wanaoishi Nairobi na ambao huishia kutumia eneo hilo limesababisha kujaa sana na kufanya iwe vigumu hata kutunza makaburi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *