Wabunge watetea hazina ya NG-CDF, wakemea wakosoaji

Martin Mwanje
2 Min Read

Wabunge ambao ni wanachama wa Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji wa Maeneo Bunge, NG-CDF wamewataka Wakenya kutetea hazina hiyo kwa udi na uvumba. 

Wamesema hazina hiyo ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu mashinani.

Mdahalo umeshamiri kuhusiana na uhalali wa hazina hiyo huku baadhi akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome wakitoa wito wa hazina hiyo kuwekwa pamoja na ile ya Magavana na badala yake kusaidia kutoa masomo bila malipo humu nchini.

Ni pendekezo ambalo wabunge hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya NG-CDF Musa Sirma ambaye pia ni mbunge wa Eldama Ravine wamepinga vikali.

Wakizungumza wakati wa utoaji wa fedha za msaada wa masomo kwa wanafunzi maskini katika eneo bunge la Dagoretti Kaskazini, wabunge hao walisema fedha hizo zimezisaidia familia maskini kulipa karo na ni muhimu katika uboreshaji wa miundombinu muhimu kote nchini.

“Sisi sote tumekusanyika hapa kunufaika kutokana na hazina hii, na unaweza ukaona bayana kile ambacho hazina hii inafanya katika uboreshaji wa miundombinu yetu ya utoaji mafunzo. Mazungumzo yoyote kuhusu kufutiliwa mbali kwa NG-CDF yana kusudi baya,” alidai Sirma.

Wakosoaji wa hazina hiyo wanadai wabunge wamekuwa wakiitumia kufuja kiasi kikubwa cha fedha hizo huku wanafunzi waliolengwa wakiambulia patupu.

Juhudi za awali za kufutilia mbali hazina hiyo hazikufanikiwa.

TAGGED:
Share This Article