Alasiri ya Jumanne Disemba 5, 2023, wabunge wa bunge la taifa waliondoka bungeni kwa ghadhabu kama njia ya kulalamikia kucheleweshwa kwa pesa za hazina ya serikali kuu ya maendeleo ya maeneo bunge NG-CDF.
Hatua yao ilisababisha kikao ambacho kilikuwa kikiongozwa na naibu spika Gladys Boss kuahirishwa hadi kesho.
Wakizungumza nje ya majengo ya bunge, wabunge hao walisema kwamba hawajapokea mgao wa fedha za hazina hiyo miezi 6 baada yao kupitisha bajeti iliyoidhinisha kutolewa kwa fedha hizo.
Walisema kile ambacho wanalilia zaidi ni pesa za kufadhili masomo almaarufu bursary ikitizamiwa kwamba wanakwenda likizo ndefu na shule zitafunguliwa mapema Januari.
Wametishia kukwamisha shughuli zote za serikali bungeni na kutokwenda likizo hadi pale ambapo fedha za hazina ya NG-CDF zitakapotolewa.
Kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi ndiye aliwasilisha hoja ya kutaka kikao hicho cha bunge kiahirishwe kwa kukosa akidi.