Chama cha wabunge wanawake hapa nchini (KEWOPA), kimeazimia kukumbatia sheria za mabunge ya kaunti kuhusu theluthi mbili ya uwakilishi sawa wa kijinsia, kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa katika bunge la kitaifa.
Wakati wa mkutano ulioandaliwa mjini Naivasha, wabunge hao wanawake walitambua ukosefu wa mikakati kuwa changamoto kuu kutekeleza usawa wa kijinsia bungeni.
Mkutano huo ulioongozwa na KEWOPA, ulilenga kubuni sheria itakayofanikisha mikakati kupitia kupitishwa kwa mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa KEWOPA ambaye pia ni mbunge wa Kajiado Leah Sankaire, alielezea umuhimu wa mfumo wa mabunge ya kaunti katika kufanikisha uwakilishi sawa wa kijinsia kwenye bunge la kitaifa. Alitoa wito kwa bunge la taifa kuiga mfumo huo.
“Tunahitaji kuiga mfano mfumo unaotekelezwa na mabunge ya kaunti, ambao ni rahisi na uliobuniwa kikatiba,” alisema Sankaire.
Aidha, wabunge hao walielezea kutoridhishwa kwao na jinsi kamati za bunge zilizvyobuniwa, wakitoa mfano na kamati kuhusu uchukuzi, ambayo ina mwanachama mmoja tu wa kike.
Ili kuhakikisha kutekelezwa kikamilifu kwa sheria ya theluthi mbili kuhusu uwakilishi wa kijinsia, KEWOPA imejitolea kuwahusisha wadau akiwemo Rais wa taifa, uongozi wa bunge, vyombo vya habari na washirika wengine muhimu.