Wabunge wahimizwa kupinga mswada wa fedha 2024

Tom Mathinji
1 Min Read
Viongozi wa upinzani wataka wabunge kupinga mswada wa fedha 2024.

Wabunge wametakiwa kupinga mswada wa kifedha wa  mwaka wa  2024, utakapowasilishwa katika bunge la taifa siku ya jumanne wiki ijayo.

Viongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, leo Ijumaa walitoa wito kwa wabunge wa mrengo huo kuhakikisha wanahudhuria kikao hicho cha bunge bila kukosa, ili kupinga mswada huo walioutaja kuwa utasababisha kupanda kwa gharama ya maisha.

Katika mkutano na wanahabari, viongozi hao walikosoa mswada huo wakisema ushuru kwenye mswada huo yatasababisha kupanda kwa bei za bidhaa za kawaida na pia kupanda kwa gharama ya maisha.

Viongozi hao wakiongozwa na Kalonzo Musyoka, Edwin Sifuna na Eugene Wamalwa, walisema wamewaandikia barua wabunge wanaounga mkono mrengo kusitisha mipango ya kusafiri na badala yake kuhudhuria vikao vya bunge la kitaifa.

Wakati huo huo, Kalonzo alikosoa makadirio ya bajeti ya shilingi trilioni  3.9 yaliyotangazwa siku ya Alhamisi akisema ni kiasi kikubwa cha fedha ambazo zinaweza kutumiwa vibaya ama kuporwa.

“Taarifa kutoka kwa waziri, katibu wa wizara na mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge lataifa, yana takwimu tofauti,” alisema Kalonzo.

Waziri wa fedha Prof. njuguna Ndung’u alisoma makadirio ya matumizi ya fedha za serikali ya shilingi trilioni 3.9 katika majengo ya bunge.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *