Wabunge wa Tanzania wapata ajali wakiwa njiani kuelekea Kenya

Basi walilokuwa wakisafiria liligongana na lori la mizigo katika maeneo ya Mbande Kongwa asubuhi ya leo Disemba 06,2024

Marion Bosire
1 Min Read

Wabunge kadhaa wa taifa jirani Tanzania waliachwa na majeraha leo wakati basi walilokuwa wakisafiria kuelekea Mombasa nchini Kenya kuhudhuria mashindano ya michezo ya mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki lilipata ajali.

Basi hilo liligongana na lori la mizigo katika maeneo ya Mbande Kongwa asubuhi ya leo Disemba 06,2024.

Taarifa rasmi kutoka bunge la Tanzania ilielezea kwamba wabunge pamoja na maafisa wanaofanya kazi bunge waliopata majeraha walipelekwa katika hospitali ya Uhuru na ile ya Benjamin Mkapa za Mkoani Dodoma.

Picha za eneo la tukio zilichapishwa kwenye akaunti rasmi ya bunge la Tanzania kwenye mtandao wa Instagram pamoja na maelezo haya, “Moja ya Mabasi yaliyokuwa yamewabeba Waheshimiwa Wabunge wanaoelekea kwenye Mashindano ya Michezo ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki limepata ajali ya kugongana na lori la mizigo maeneo ya Mbande Kongwa asubuhi hii. Majeruhi wa ajali hiyo wamekimbizwa Hospitali ya Uhuru na Hospitali ya Benjamini Mkapa za Mkoani Dodoma.”

Mbunge wa eneo la Alego Usonga nchini Kenya Samuel Atandi alithibitisha ajali hiyo katika kituo cha reli ya kisasa cha Nairobi walipokuwa wakiabiri Treni kuelekea Mombasa kwa ajili ya michezo hiyo.

Atandi aliwatakia afueni ya haraka wenzao wa Tanzania kutokana na hilo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *