Wabunge wa ODM wazungumzia suala kutenga maeneo ya uwaniaji

Wanahimiza makubaliano kuhusu jinsi ya kugawana maeneo ya uwaniaji na chama tawala UDA ambacho sasa wanashirikiana nacho.

Marion Bosire
2 Min Read

Viongozi wa chama cha Orange Democratic Movement, ODM, wameonyesha kutoridhika na taarifa kwamba uongozi wa chama cha United Democratic Alliance, UDA, unapanga kuwasilisha wawaniaji katika maeneo ambayo ODM ina uungwaji mkono kama Nyanza, eneo la Magharibi na Pwani.

Wakihutubia wanahabari, viongozi wa ODM wakiongozwa na Mbunge wa eneo la Suba Kaskazini Millie Odhiambo walisema kwamba iwapo chama kitakubaliana na chama tawala kuhusu kutenga maeneo fulani, hayo yatakubalika kwa viongozi na hata wapiga kura.

Wabunge hao wanachama wa ODM wanataka uongozi wa chama ushughulikie suala hilo ambalo kulingana nao linatishia kusambaratisha mpango wa serikali jumuishi iwapo utatekelezwa mwaka 2027.

Wanasisitiza kwamba uchaguzi unastahili kuwa huria katika maeneo ambapo sio ODM pekee inayoweza kuwasilisha wawaniaji ila pia vyama vingine kote nchini, uchaguzi unapokaribia.

Viongozi hao walisema kwamba uteuzi unafaa kuwa suluhisho kwa suala na kutenga maeneo iwapo hautakuwa ukidunisha mfumo wa vyama vingi.

Uongozi wa ODM vile vile unataka mpango wa kugawana mamlaka nusu kwa nusu na wapatiwe wadhifa wa Naibu Rais huku mazungumzo ya kubuni muungano na chama tawala yakitarajiwa kuandaliwa.

Suala la jinsi wawaniaji wa ODM na UDA watapeana nafasi wakati wa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027 limekuwa likikanganya wafuasi wa vyama hivyo huku wadadisi wakionya kwamba huenda likahujumu mpango wa serikali jumishi.

Share This Article