Wabunge na Maseneta kadhaa wameelezea kukatalia mbali nyongeza ya mshahara iliyopendekezwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC.
Miongoni mwao ni mbunge wa Saboti Caleb Amisi ambaye amemwandikia barua karani wa Bunge la Taifa akiashiria kuwa kamwe hataki nyongeza ya mshahara.
“Naandika kukataa rasmi ongezeko la hivi mazu la mshahara lililotolewa kwa wabunge. Ikizingatiwa hali ya sasa ya kiuchumi na gharama ya juu ya maisha inayowakumba Wakenya wengi nchini mwetu, ninaamini ni bora kwetu kuonyesha uwajibikaji wa kifedha na umoja na wakazi wa maeneo bunge yetu,” alisema mbunge huyo katika barua iliyoandikwa leo Jumatano.
“Badala ya kukubali kuongezwa mshahara, naelekeza kuwa fedha hizo zitumiwe kufadhili mpango wa msaada wa masomo ndani ya eneo bunge langu. Mpango huu hususan utawalenga wanafunzi wenye changamoto za kifedha wanaohitaji msaada wa masomo.”
Mbunge wa Kisumu Central Joshua Oron pia amekatalia mbali nyongeza hiyo akisema fedha hizo badala yake zitumiwe kutekeleza miradi ya maendeleo itakayowanufaisha raia.
“Nataka ibainike kwamba nimekataa ongezeko la mshahara linalodaiwa kupendekezwa na SRC na kuitaka tume hiyo kuelekeza fedha hizo kwa masuala mengine yanayolikumba taifa kama vile malipo ya walimu wa JSS na pia madaktari wanagenzi,” alisema Oron.
Katika bunge la Seneti leo Jumatano, Maseneta kadhaa walimkemea mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich kwa kile walichokitaja kuwa njama ya kutaka kuwakosanisha na Wakenya kwa kupendekeza waongezewe mshahara wakati huu ambao nchi inakabiliwa na changamoto si haba.
Maseneta Edwin Sifuna wa Nairobi, Enock Wambua wa Kitui na Samson Cherargei wa Nandi ni miongoni mwa Maseneta waliopuuzilia mbali pendekezo la SRC wakisema hawakuomba kuongezewa mshahara.
Ikiwa pendekezo la SRC la litatekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 ulioanza Julai Mosi mwaka huu, basi mshahara wa Maspika wa bunge la Taifa na Seneti utaongezwa hadi shilingi 1,208,362 kutoka shilingi 1,185,327, ya Mawaziri na Magavana itaongezwa hadi shilingi 990,000 kutoka shilingi 957,000 huku mshahara wa Naibu Spika ukiongezwa hadi shilingi 966,690 kutoka shilingi 948,261.
SRC pia imependekeza kuongezwa kwa mshahara wa Makatibu kutoka shilingi 792,519 hadi 819,844, viongozi wa walio wengi na wachache kutoka shilingi 784,768 hadi 800,019, Wabunge na Maseneta kutoka shilingi 725,502 hadi shilingi 739,600 huku tume hiyo ikipendekeza mshahara wa Wawakilishi Wadi kuongezwa kutoka shilingi 154,481 hadi shilingi 164,588.