Wabunge 6 wa ODM kuchukuliwa hatua kwa kuunga mkono mswada wa fedha

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha upinzani nchini Kenya, Orange Democratic Movement – ODM sasa kinasema kwamba kitaanzisha taratibu za kuwaondoa kazini wabunge sita wa chama hicho.

Adhabu hiyo imechochewa na hatua ya sita hao ya kuunga mkono mswada wa fedha wa mwaka 2024 ulipokuwa ukipigiwa kura bungeni kinyume na msimamo wa chama.

Kulingana na taarifa wabunge hao ni Elisha Odhiambo wa Gem, Gideon Ochanda wa Bondo, Emmanuel Wangwe wa Navakholo, Elijah Kanchory wa Kajiado ya kati, Bernard Shinali wa Ikolomani na Caroli Omondi wa Suba Kaskazini.

Katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna alihutubia wanahabari leo baada ya mkutano wa kamati kuu ya chama, ambapo alisema kwamba wabunge hao walikosa kutumiza masharti ya viapo walivyokula kwa kutozingatia matakwa ya watu wa maeneo yao.

Kuhusu kisa cha waandamanaji kuingia bunge wiki iliyopita, Sifuna alisema ni sawa na kura ya kutokuwa na imani katika uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza.

Alimtaka Rais William Ruto na serikali yake kuzingatia matakwa ya wakenya wanaotekeleza maandamano nchini.

Sifuna alilaani hatua ya maafisa wa polisi ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na visa vya kutekwa nyara kwa baadhi ya waandamanaji.

Seneta huyo wa kaunti ya Nairobi anataka pia kwamba serikali kuu iwajibikie matukio ya maandamano kama vile vifo, majeraha na uharibifu wa mali.

Wakati huo huo alipongeza wakenya hasa vijana kwa kudhihirisha umoja kufuatia mchango wa haraka na wa pesa nyingi wa kugharamia matibabu ya waliojeruhiwa wakati wa maandamanao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *