Waandalizi wa shindano la ndondi kati ya wanamuziki wa Nigeria Portable na Speed Darlington la Aprili 18, 2025 wameonywa.
Shirikisho la kitafa la ndondi nchini Nigeria NBF limechukua hatua hiyo kufuatia kutofahamika kwa hali ya afya ya wawili hao na muda mfupi uliotolewa kwao kujiandaa.
Onyo hili linajiri wiki moja tu baada ya Olusegun ‘Success’ Olanrewaju kuzirai na kufariki katika pigano la ndondi nchini Ghana. Ripoti zinaashiria kwamva Sucess alifariki kutokana na mshtuko wa moyo.
Rais wa muda wa NBF Azania Omo-Agege, amewasihi waandalizi wa pigano hilo watangulize usalama kabla ya pigano lenyewe.
Huku akifurahikia uhamasisho kuhusu mchezo wa ndondi, Omo-Agege aliwataka waandalizi pia wahakikishe wanafahamu hali ya afya ya wanamuziki hao.
“Hawa ni wanamuziki huwa sihusiki nao sana, lakini nina uhakika wanatumia pombe na hivyo iko kwenye miili yao.” alisema mkuu huyo wa NBF akitilia shaka ufaafu wao hasa ndani ya muda wa wiki mbili pekee.
“Ninashauri waandalizi pia wahakikishe kwamba zamu hii, Portable na Speed Darlington wanavaa kofia za kukinga vichwa vyao.” aliendelea kusema.
Portable aliwahi kuhusika kwenye pigani jingine na mwigizaji wa Nollywood Charles Okocha mwaka 2023 na hawakuwa wamevaa kofia hizo na Portable ndiye aliibuka mshindi.
Uhasama kati ya Portable na Speed Darlington uliongezeka baada ya Darlington kumwalika Portable kwa hafla yake na kuahidi kumlipa Naira laki tano, kiasi cha pesa ambacho kilimghadhabisha Portable.
Portable ameonekana akifanya mazoezi kabla ya shindano hilo.