Shirikisho la soka barani Afrika, CAF linatarajiwa kutangaza waandalizi wa fainali za kombe la bara Afrika miaka ya 2025 na 2027 kwenye mkutano utakaoandaliwa leo jijini Cairo, Misri.
Kenya ni baadhi ya mataifa ambayo yanasubiri tangazo hilo kwa hamu na hamumu baada ya kuwasilisha ombi la kuandaa makala ya mwaka 2027 pamoja na Uganda na Tanzania.
Kenya imeorodhesha viwanja vya Nyayo, Kasarani na Kipchoge Keino, ilhali Uganda inanuia kuandaa fainali hizo katika viwanja vya Nelson Mandela, Nakivubo, Akii Bua na Hoima.
Tanzania imewasilisha viwanja vya Benjamin Mkapa, CCM Kirumba, Jamuhuri, Sheikh Amri Abeid na Amani.
Mataifa hayo matatu hata hivyo yatapata upinzani kutoka kwa Nigeria na Benin ambayo yamewasilisha ombi la pamoja la kuandaa mashindano hayo ilhali Algeria ilijiondoa Jumanne iliyopita.