Vybz Kartel kutumbuiza Uganda mwezi Mei

Ameorodheshwa kama mtumbuizaji mkuu wa awamu ya kwanza ya tamasha ya Talanta Afrika Mashariki.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa Dancehall kutoka Jamaica Adidja Azim Palmer, maarufu kama Vybz Kartel, atakuwa mtumbuizaji mkuu katika tamasha ya Talanta nchini Uganda.

Hiyo itakuwa awamu ya kwanza kabisa ya tamasha hiyo ya Talanta Afrika Mashariki na waandaaji wameahidi kuwa na onyesho la kipekee.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha hiyo katika mkahawa wa Lugogo jijini Kampala, waandalizi walitaja Mei Mosi, 2026 kuwa tarehe ya tukio hilo.

Vybz Kartel ndiye mtumbuizaji mkuu akifuatiwa na watumbuizaji kadhaa wa eneo zima la Afrika Mashariki.

Wasanii wa Uganda waliothibitishwa kuingia jukwaani siku hiyo ni pamoja na Elijah Kitaka, Aaron X, Cindy Sanyu, DJ Litto, Etaniah na wapiga muziki Roja & Slick Stuart.

Mtayarishaji muziki ambaye pia husimamia wasanii nchini Uganda George Kagoda almaarufu Bushingtone ndiye aliyekuja na wazo la tamasha hiyo.

Mwongoza hafla Edwin Katamba maarufu kama MC Kats, alielezea kwamba wazo hilo lilijiri baada ya Kagoda kushangaa ni kwa nini wasanii wa Afrika Mashariki huwa hawahusishwi kwenye matamasha ya kimataifa.

Alitaja matamasha kama Summerfest, Coachella na Afro Nation, ambapo Kats anakubaliana kwamba eneo hili linahitaji tamasha ya kiwango cha tamasha ya kimataifa.

Bushingtone anasema kwamba lengo la tamasha hiyo kubwa ni kusherehekea muziki wa Afrika Mashariki na utamaduni huku ikijenga soko thabiti la kieneo la burudani.

Share This Article