Vyama vya wafanyakazi wa sekta ya umma vimesitisha mgomo ulioitishwa kulalamikia sintofahamu kwenye mpito kutoka kwa hazina ya kitaifa ya bima ya afya NHIF hadi mpango wa halmashauri ya afya ya jamii SHA.
Hii ni baada ya viongozi wa vyama hivyo kuafikia makubaliano na serikali.
Viongozi hao walikubali kusitisha mgomo baada ya kutia saini makubaliano na mawaziri Justin Muturi wa utumishi wa umma, Alfred Mutua wa leba na Debra Mulongo Barasa wa Afya katika jumba la Harambee jijini Nairobi.
Katibu mkuu wa chama cha watumishi wa umma Tom Odege alisema kwamba sio nia yao kuitisha migomo, lakini wanafanya hivyo ili mwajiri ashughulikie wasiwasi wao.
“Serikali sasa imejibu na tunasitisha mgomo.” alisema Odege.
Kulingana naye bima ya afya ni muhimu kwa wanachama wa vyama vyao na kwamba wanatarajia mazuri kutoka kwa bima mpya ya afya hata baada ya changamoto kushuhudiwa wakati wa kuizindua.
Katika ilani ya mgomo ya siku 14 waliyotoa Oktoba 8, 2024, viongozi hao wa vyama vya wafanyakazi waliibua maswali kuhusu mpito wa NHIF hadi SHA bila bima pana kwa watumishi wa umma.
Waligusia pia hatima ya wafanyakazi wa NHIF na ongezeko la ada za kila mwezi hadi asilimia 2.75 ya mishahara bila masharti bora kwa wanachama wao.
Serikali imekubaliana na vyama hivyo vya wafanyakazi wa sekta ya umma kwamba wizara ya utumishi wa umma itaendeleza bima pana ya watumishi wa umma hadi Novemba 21, 2024 kupitia SHA, ambayo imechukua majukumu ya NHIF.
Makubaliano yaliyotiwa saini aisha yanasema kwamba watumishi wa umma wataafikia huduma bora hata baada ya Novemba 21, 2024.
Walikubaliana pia kwamba kamati ya muda ibuniwe ili kuhakikisha mpito kamili wa wafanyakazi wa NHIF hadi SHA kulingana na sheria ya SHA ya mwaka 2023, Sheria ya ajira ya mwaka 2007, Sheria ya Leba na makubaliano ya pamoja.
Waziri Muturi alishukuru viongozi wa vyama hivyo vya watumishi wa umma kwa uelewa na mchango wao uliofanikisha makubaliano ya leo.
Waziri Alfred Mutua wa Leba kwa upande wake alitaka mzunguko wa makabiliano ukome kila kunapozuka mzozo.
Waziri Barasa alihakikishia wakenya kujitolea kwa serikali kutoa huduma za afya za gharama nafuu, faafu na zinasopatikana.