Msajili Mkuu wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya kisiasa kuzingatia kanuni za maadili ya vyama ,ili kukuza uhusiano mwema na uchangamano kati ya vyama na kwa wanachama .
Akizungumza wakati wa kufungua ofisi mpya ya kusajili vyama mjini Bungoma, Bi Nderitu alibainisha kuwa kanuni hizo zinakataza vurugu za kisiasa ndani ya vyama vya siasa na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani.
Msajili huyo alisema kuwa kanuni za vyama huwapa wanachama fursa ya kutoa maoni yanayohusu vyama vyao na pia nafasi ya kufahamu utendakazi wa viongozi.
Nderitu alitoa wito wa kuheshimiwa kwa haki za binadamu na uhuru wa kimsingi kwa kila mtu binafsi na wale kutoka makundi maalum kama wanawake na walemavu.
Alisisitiza haja ya kuzingatiwa na kuheshimiwa kwa utawala wa sheria katika kukuza umoja wa kitaifa kwa njia ya mazungumzo, akisema kwamba wakati wowote kunapotokea suala ni muhimu pande zinazohusika ziwe na mazungumzo ya kutafuta suluhu
Nderitu alisema kuwa kufunguliwa kwa ofisi hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanachama wa vyama vya siasa wanafahamu kinachoendelea katika vyama vyao.
Msajili huyo wa vyama aliwataka wananchi kutambua kuwa wako huru kujiunga na chama chochote cha kisiasa,akifichua kuwa kwa sasa kuna wanachama wapatao milioni 24 waliosajiliwa wa vyama vya siasa.
Ofisi hiyo mpya itatumikia maeneo ya Bungoma, Busia na Kakamega.