Shughuli za kawaida leo Jumatano zilisitishwa katika soko la Dagoretti baada ya vita kuzuka kati ya wafanyabiashara na kundi la vijana wanaokisiwa kuwa walanguzi wa mihadarati sehemu hiyo.
Wafanyabiashara hao wanaomba maafisa wa usalama kutoka upande wa Kikuyu, kaunti ya Kiambu na wenzao wa Dagoretti Kusini, kaunti ya Nairobi kushirikiana ili kumaliza makundi ya walanguzi wa mihadarati wanaowahangaisha wakazi.
Vita hivyo vinasemekana kuzuka baada ya kuzorota kwa hali ya usalama eneo hilo ambapo Jumapili iliyopita, genge hilo la vijana lilidaiwa kumvamia kijana mmoja wakati wa mchana na kumwangamiza.
Kwa sasa, wafanyabiashara wametoa makataa ya saa ishirini na nne kubomolewa na kuondolewa kwa biashara hizo za mihadarati la sivyo wataendelea kukambiliana nao vilivyo ili kuwaangamiza.
Hali ya mshikemshike ingali inaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo huku wananchi wakikabiliana na maafisa wa usalama wanaotumia vitoa machozi kuwatuliza.