Vituo vyote vya kujaza gesi vilivyo ndani ya mita 200 kutoka eneo la makazi kuanzia sasa vitafungwa.
Hayo yamesemwa na Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja leo Jumanne alipotembelea familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye mkasa wa moto uliotokea eneo la Mradi katika eneo bunge la Embakasi Mashariki wiki jana.
Amesema uamuzi huo umefikiwa kwa makubaliano na mamlaka ya udhibiti wa bidhaa za petroli nchini, EPRA.
“Tumekubaliana na EPRA na kuelekeza kuwa vituo vyote vya kujaza gesi vilivyo ndani ya mita 200 kutoka eneo la makazi vifungwe kuanzia sasa,” alisema Sakaja ambaye pia alitembelea kituo cha afya cha Embakasi na hospitali ya Mama Lucy wanakoendelea kutibiwa waathiriwa wa mkasa wa mlipuko wa gesi katika eneo la Mradi.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametaka kila familia iliyoathiriwa na mkasa huo kulipwa fidia ya shilingi 500,000.
Waathiriwa wa mkasa huo wamekuwa wakipokea usaidizi wa kila aina kutoka kwa serikali ikiwa ni pamoja na kupewa bidhaa muhimu za matumizi ya kila siku.
Washukiwa wanne wanaohusishwa na mlipuko huo walifikishwa katika mahakama moja ya Milimani leo Jumanne.
Wanne hao ni Derrick Kimathi ambaye ni mmiliki wa kituo hicho cha kuuza gesi pamoja na David Ongare, Joseph Makau na Marrian Kioko ambao ni maafisa wa halmashauri ya usimamizi wa mazingira, NEMA.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama iwazuilie washukiwa hao ili kuwapa maafisa wa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi. Kimathi alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi baada ya kujisalimisha jana Jumatatu.
Idara ya DCI imesema bado inawatafuta washukiwa wengine watano.