Ukraine imeonya kuwa tayari inalazimika kupunguza baadhi ya operesheni za kijeshi kwa sababu ya kupugua kwa misaada ya kigeni.
Jenerali mkuu Oleksandr Tarnavskyi alisema wanajeshi walikabiliwa na uhaba wa risasi kwenye “mstari wa mbele kabisa”, na kusababisha “tatizo kubwa” kwa Kyiv.
Haya yanajiri wakati mabilioni ya dola ya misaada ya Marekani na EU yamezuiliwa huku kukiwa na mizozo ya kisiasa.
Ukraine ilisema inatumai kuongeza hifadhi yake ya risasi kwa usaidizi wa magharibi.
Lakini inategemea sana vifaa vya magharibi, haswa juu ya uwasilishaji wa makombora ya masafa marefu na mifumo ya ulinzi wa anga, ili kupigana na majeshi ya Urusi.
Jenerali Tarnavskyi aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba nchi hiyo haikuwa na makombora ya mizinga, haswa kwa silaha zake za enzi ya Soviet.
“Kiasi tulichonacho hakitoshi, kwa kuzingatia mahitaji yetu,” alisema. “Kwa hivyo, tunazisambaza upya”.