Serikali nchini Tanzania imetangaza bei mpya ya juu ya mafuta inayoanza kutekelezwa hii leo Jumatano, tarehe mosi, Aprili 2026.
Kulingana na Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania EWURA, kupanda kwa bei hizo kumetokana na ongezeko kubwa linalosababishwa na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati dhidi ya Iran.
Bei ya lita ya petroli jijini Dar es Salaam imepanda kwa shilingi 956 za Tanzania ambayo ni sawa na dola senti 37 na kuzua hisia kali miongoni mwa raia wa taifa hilo.
Kwa mujibu wa bei mpya mjini Dar es Salaam, petroli sasa itauzwa kwa shilingi za Tanzania 3,820, dizeli Sh 3,806 na mafuta ya taa Sh 3,684.
Mjini Tanga, petroli itauzwa kwa shilingi 3,881, dizeli shilingi 3,867 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa shilingi 3,745.
Mjini Mtwara, petroli itauzwa kwa shilingi 3,912, dizeli shilingi 3,898, mafuta ya taa shilingi 3,777 huku maeneo mengine petroli ikiwa ni zaidi ya shilingi 4000.
Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania na mchumi Zitto Kabwe ameitaka serikali kuwasaidia wananchi kubeba mzigo huo wa mafuta.
Katika chapisho lake la mtandao wa X zamani Twitter, Kabwe amesema:
‘Leo tumeamka na bei mpya ya mafuta, bei tuliyoitegemea kufuatia mashambuliizi yanayoendelea ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Kama ilivyo sehemu zote duniani bei imepanda sana na gharama za maisha zitakuwa kubwa sana. Serikali isaidiane na wananchi kubeba gharama hizi.”
Kulingana na Ewura, mashambulizi katika visima vya mafuta, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta katika eneo la Mashariki ya Kati pamoja na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz unaopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote duniani ndio sababu inayochangia kupanga kwa gharama ya uagizaji wa bidhaa hiyo nchini Tanzania.
Taarifa ya Abdalla Seif Dzungu, BBC Swahili, Nairobi Kenya