Mamia ya watu wameandamana katika Ukanda Gaza, wakitaka kukomeshwa kwa vita na Hamas kujiuzulu kutoka madarakani.
Hayo ni maandamano makubwa zaidi dhidi ya vuguvugu la Wapalestina linalodhibiti ukanda huo kuwahi kushuhudiwa tangu vita vilipoanza Oktoba 7, 2023.
Waandamanaji walikusanyika karibu na kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Beit Lahia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na kisha kuandamana kupitia barabara zilizozingirwa na vifusi vya majengo na nyumba zilizoharibiwa wakati wa vita, karibu na Hospitali ya Indonesia.
Nao waliimba nyimbo na kutoa kauli ikiwemo “Hamas out, out,” kulingana na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Wanachama wa Hamas waliojifunika nyuso zao, baadhi wakiwa na silaha na wengine wakiwa wamebeba marungu, waliwatawanya waandamanaji kwa nguvu na kuwashambulia baadhi yao.
Kulingana na BBC, Hamas hawakutoa maoni yao mara moja kuhusu maandamano hayo, lakini wafuasi wa vuguvugu hilo walipuuza umuhimu wake.