Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo ameapa kuwa Kenya haitalegeza kamba katika kukabiliana na ugaidi na mashambulizi yanayotokana na itikadi kali.
Dkt. Omollo ameelezea namna taifa hili linavyoendelea kukabiliwa na matishio ya ugaidi na mashambulizi yanayotokana na itikadi kali akisisitiza umuhimu wa tahadhari kuchukuliwa wakati wote.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa Kenya haigeuki kuwa maficho ya magaidi au shughuli za itikadi kali,” alisema Katibu huyo wakati wa kongamano kuhusu Mswada wa Mpango wa Uzuiaji wa Mashambulizi Yanayotokana na Itikadi Kali (PVE) lililoandaliwa kwa ajili ya serikali za kaunti katika hoteli moja mjini Naivasha.
Alipongeza mswada huo akiutaja kuwa hatua muhimu katika kukabiliana na mashambulizi yanayotokana na itikadi kali.
Aidha aliuelezea kama mpangokazi unaozipa kaunti vifaa vya kukabiliana ipasavyo na uovu huo katika mifumo yao ya uongozi, ufadhili wa mpango huo na kukuza ushirikiano kati ya serikali kuu na zile za kaunti.
Katibu Omollo alisema serikali imekusudia kukuza umoja wakati ikihakikisha usalama wa nchi na kutoa wito kwa washikadau wote kufanya kazi pamoja kutekeleza mswada huo na kupambana na mashambulizi yote yanayotokana na itikadi kali.