Vita dhidi ya ufisadi: Rais Ruto atema cheche

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto amesema hakuna asasi ya serikali itakayosazwa katika vita dhidi ya ufisadi. 
Isitoshe, amesema yuko tayari kuongoza jitihada za kupigana dhidi ya uongozi mbaya, maslahi ya kibinafsi na ufisadi ili kuleta mabadiliko nchini.
Ameahidi kupigana dhidi ya maovu hayo matatu bila kujali ikiwa yamejikita katika serikali kuu, bunge au idara ya mahakama huku akiyataja kuwa kikwazo kwa juhudi za kuleta mabadiliko nchini.
Kulingana naye, Wakenya wamepoteza subira na wana shauku ya kuona mabadiliko yanayoathiri maisha yao moja kwa moja yakitekelezwa.
“Tutafanya kila tuwezalo kupigana na ufisadi,” alisema kiongozi wa nchi leo Jumatano wakati akiwa mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia.
Katika siku za hivi karibuni, Rais Ruto amelalamikia tabia ya watu fulani kukimbilia mahakamani kupinga utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya serikali.
Ametoa mfano wa mpango wa nyumba za bei nafuu na upatikanaji wa afya kwa wote, miradi ambayo anasema itaendelea kutekelezwa na liwe na liwalo licha ya kupingwa mahakamani.
Rais akiilaumu idara ya mahakama kwa kushirikiana na watu hao kuhujumu utekelezaji wa miradi ya serikali, akihusisha kutolewa kwa maagizo ya kuzuia utekelezaji wa miradi hiyo na kukithiri kwa ufisadi katika idara ya mahakama.

“Badala ya kuhongana kortini, tutamaliza ufisadi kortini,” aliapa Rais Ruto wakati akizindua ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika eneo la Soy, kaunti ya Uasin Gishu jana Jumanne.

“Ati kuna watu wengine wananiambia ati kwa sababu ile serikali ilipita, ati walikuwa na budget ya kuhongana kortini, ati mimi niende nitengeneze budget ya kuhongana kortini. Mnataka ati pesa yenu itumike kuhongana kortini? Hiyo kazi haiwezi bwana, haiwezekani. Hakuna budget itatengenezwa ya kuhonga mtu yeyote kortini.”

Hata hivyo, taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tume ya Huduma za Mahakama, JSC, Chama cha Majaji na Mahakimu na LSK sawia na mashirika mbalimbali ya kijamii zimeelezea kutoridhishwa na matamshi ya Rais zikionya kuwa yanaweza yakasababisha kutoheshimiwa kwa idara ya mahakama na kuwa chanzo cha uvunjaji wa sheria.

Share This Article