Vita dhidi ya pombe haramu vyachacha Kericho

Martin Mwanje
2 Min Read

Kamishna wa kaunti ya Kericho Gilbert Kitiyo amewaagiza maafisa wa polisi kuimarisha msako dhidi ya pombe haramu zikiwemo baa zinazouza pombe hiyo. 

Kitiyo ameonya kuwa maafisa wa usalama watafanya msako mkali dhidi ya pombe haramu  kaunti ndogo zote sita katika kaunti ya Kericho hadi uovu huo utakapoangamizwa na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Huku akisema unywaji pombe haramu ni hatari kwa afya na unaweza ukasababisha hata maafa, Kamishna huyo aliwaomba vijana kuwachana na matumizi ya dawa za kulevya akisema zitaharibu maisha yao.

“Inahuzunisha sana kuona watu wengi wakifa kutokana na unywaji wa pombe haramu katika Kaunti ya Kirinyaga na ndiyo maana hapa Kericho hatutaki kisa kama hicho kitokee,” alisema Kitiyo

Wakati huo huo, alionya kuwa wanaoendesha mchezo ulioharamishwa wa kamari katika kaunti ya Kericho hawatasazwa kwani polisi watachukuwa mashine zao kwa lazima na kuzichoma kwa kuwa zimeletea familia nyingi umaskini.

“Mashine za kuchezea kamari hazijapewa leseni ya kufanya kazi popote pale, na zile zinazodai kuwa na leseni ni bandia. Ni mashine za bei ghali, lakini tutaendelea kuziharibu hadi uovu huo ukomeshwe katika Kaunti yetu,” alisisitiza Kitiyo.

Kamishna huyo alikuwa akizungumza katika soko la Kapkatet, kaunti ndogo ya Bureti ambapo aliwaomba wakazi kuwa macho na kuripoti visa vya uhalifu kwa polisi ili wanaotekeleza visa hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Share This Article