Visa vya ukeketaji wa wanawke nchini Kenya vinaendelea kupungua kwa taratibu.
Utafiti wa shirika la demografia na afya nchini uliofanywa mwaka wa 2022 unaonyesha kuwa visa vya ukeketaji vilipungua kutoka asilimia 21 mwaka wa 2014 hadi asilimia 15 mwaka wa 2022.
Kulingana na Katibu anayehusika na masuala ya jinsia Ann Wang’ombe, mila hiyo kandamizi imekuwa ikiibua changamoto nyingi kwa vile ukeketaji umejikita sana katika mila za kitamaduni na mara nyingi hufanywa kisiri.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha Siku ya kKimataifa ya Mtoto wa Kike katika eneo la Elangata Wuas, kaunti ya Kajiado Wang’ombe, alielezea matumaini yake kuwa mila hiyo iliyopigwa maarufuku itatokomezwa kabisa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kutokana na kampeni kali na juhudi za uhamasishaji dhidi yake.
“Visa vya ukeketaji wanawake vimepungua katika muda wa miaka kadhaa iliyopita, na tuna uhakika kwamba katika muda wa miaka miwili ijayo, vitakuwa vimemalizwa kikamilifu,” alisema Wang’ombe.
Alizitaka jamii zinazoendeleza ukeketaji kuzingatia kanuni mbadala za mpito ambazo zitawaruhusu wasichana kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
Wang’ombe alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya wadau wote ili kutokomeza ukeketaji hasa shule zinapofunga kwa likizo ndefu, wakati ambapo vitendo hivyo hukithiri.