Uganda imethibitisha visa viwili zaidi vya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox na kufanya idadi ya visa nchini humo kufikia vinne kulingana na wizara ya afya.
Wagonjwa hao wawili wapya waliambukizwa aina ya virusi vya clade 1b, kulingana na mkurugenzi mkuu wa huduma za afya Henry Mwebesa.
Visa hivyo viwili vilithibitishwa wiki hii, mwathiriwa wa kwanza akiwa dereva wa malori ya masafa marefu, huku maelezo kuhusu mwathiriwa wa pili yakikosa kutolewa.
Shirika la Afya Ulimwenguni lilitangaza mlipuko wa hivi majuzi wa ugonjwa huo kuwa dharura ya afya ya umma baada ya kuzuka kwa aina mpya ambayo inaenea kwa haraka.
Maafisa wa afya nchini Uganda waliripoti kwa mara ya kwanza kuzuka kwa ugonjwa huo nchini humo mnamo Julai 24 mwaka huu.