Wabunge wanaoegemea muungano unaotawala wa Kenya Kwanza wametetea maafikio ya serikali wakisema nchi iko katika mkondo sawa chini ya uongozi wa Rais William Ruto.
Wakiongozwa na mbunge wa kaunti ya Kiambu Ann Wamuratha, mwenzake wa Narok Rebecca Tonkei na mwakilishi wa Kenya katika bunge la Afrika Mashariki David Sankok viongozi hao walisema serikali ya Ruto imepiga hatua.
Wamuratha alisema hivi karibuni wakenya watafahamu kwamba Ruto ana nia nzuri na ifikapo mwaka 2027 atachaguliwa tena kwani uchumi wa Kenya utakuwa umefika ulipofikia wakati wa Rais Kibaki.
Kuhusu vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya, viongozi hao walipongeza oparesheni inayoendeshwa na serikali ya kitaifa dhidi ya vileo ambavyo vimesumbua wengi.
Akizungumza kwenye mkutano kuhusu usaidizi wa kimasomo almaarufu “Mama County Scholarship program”, Tonkei alipongeza hatua ya serikali ya kuajiri walimu zaidi ili kukidhi uhaba uliopo hasa katika kaunti zilizotengwa.
Kiongozi huyo alidai kwamba kwa sasa hakuna upinzani Kenya kufuatia hatua ya Rais ya kuunga mkono azma ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ya kuwania uenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika.
Sankok alipongeza hazina ya NGAAF kwa kuafikia hatua ya kuwezesha jamii hata ingawa imetengewa shilingi milioni 53 pekee kwa bajeti ya kila mwaka.
Alikariri maoni ya Tonkei kuhusu uwaniaji wa Raila Odinga wa uenyeketi wa tume ya AU akisema ataunganisha bara Afrika iwapo atachaguliwa.